Raisi Wa Marekani Asema Nchi Yake Kuwa Na Wagonjwa Wengi Wa Corona Ni Heshima

Rais Donald Trump amesema ni '' ni heshima '' kuwa Marekani ina idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona duniani.
''Ninalitazama suala hili kama heshima fulani, kama jambo zuri kwasababu inamaanisha kuwa vipimo vyetu viko vizuri,'' alieleza akiwa Ikulu ya Marekani.
Marekani ina watu milioni 1.5 walioathiriwa na virusi vya corona na karibu vifo 92,000, kwa mujibu wa takwimu zinazokusanywa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins. Nchi inayoshika nafasi ya pili ni Urusi ikiwa na maambukizi ya watu 300,000.

Aliwaambia waandishi wa habari, ''unajua unaposema kuwa tunaongoza kuwa na watu wengi walioambukizwa, ni kwa sababu tuna vipimo vingi kuliko mtu mwingine yeyote.''
''Hivyo tuna watu wengi walioambukizwa,'' aliendelea, ''Sitazami kama jambo baya, ninalitizama kwa heshima fulani, kama jambo jema kwa sababu ina maanisha kuwa tuna vipimo vizuri.''
Aliongeza: ''Hivyo ninaliona kama nembo ya heshima. Kweli ni heshima.
''Ni heshima kwa vipimo na kazi ambayo wataalamu wameifanya.''
Kwa mujibu wa kituo cha kupambana na kudhibiti magonjwa , Marekani imepima watu milioni 12.6 mpaka siku ya Jumanne.


EmoticonEmoticon