Visa Vya Corona Nchini Kenya Vyafikia 607

Kenya imesajili visa 25 zaidi vya maambukizi ya virusi vya corona na kufikisha idadi ya jumla ya watu 607 waliothibitishwa kuambukizwa virusi hivyo.

Katibu msimamizi katika wizara ya Afya Rashid Aman alisema kwamba kati ya 25 hao wakenya ni 22, Tanzania mmoja, Uganda mmoja na Uchina mtu mmoja.

Nairobi iliongoza kwa jumla ya watu 17 waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya corona katika muda wa chini ya saa 24, huku kaunti ya Isiolo ikiwa kaunti ya hivi punde kusajili kisa cha corona kufikisha 18 kaunti ambazo zimesajili maambukizi ya corona kote nchini. 

Mtaa wa Eastleigh katika kaunti ya Nairobi umesajili visa tisa ya maambukizi.

Aman alitangaza kwamba watu watatu zaidi wamefariki kutokana na virusi vya corona katika kipindi cha chini ya saa 24 zilizopita na kufikisha idadi ya walioaga dunia kutokana na covid 19 humu nchini hadi watu 29. 

 Aman pia alisema jumla ya watu 197 wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya watu saba zaidi kupona ugonjwa huo katika muda wa saa 24 zilizopita.
credit:radiojambo


EmoticonEmoticon