Maandamano Makubwa Ya Kupinga Ubaguzi Yafanyika Marekani


Maandamano makubwa ya amani yamefanyika kote nchini Marekani kupinga ubaguzi wa rangi na unyanyasaji unaotekelezwa na maafisa wa polisi ikiwa ni siku ya 12 ya maandamano yaliosababishwa na kifo cha George Floyd.

Makumi ya maelfu ya watu waliandamana mjini Washington DC ikiwa ndio maandamano makubwa kufanyika katika mji huo kufikia sasa.

Makundi ya watu pia yaliandamana mjini New York, Chicago, LA na San Fransisco. Wakati huohuo , watu walitoa heshima zao kwa Floyd katika jimbo la North Carolina, ambapo alizaliwa kabla ya ibada ya kumbukumbu yake kufanywa.

Bwana Floyd mtu mweusi ambaye alikuwa hana silaha , alifariki katika mikono ya polisi katika mji wa Minneapolis tarehe 25 mwezi Mei. 

Picha ya video ilimuonesha afisa wa polisi ambaye ni mzungu akiwa ameweka goti lake kwenye shingo ya Floyd kwa zaidi ya dakika tisa akiwa amekandamizwa barabarani.

Afisa wa polisi Derek Chauvin amefukuzwa kazi na kushtakiwa kwa kutekeleza mauaji. Maafisa wengine watatu ambao walikuwepo katika eneo hilo pia walifutwa kazi na kushitakiwa kwa kusaidia na kuunga mkono kilichokuwa kikiendelea.

Maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi wa rangi pia yalifanyika katika baadhi ya mataifa mengine. 

Nchini Uingereza, katika bustani ya bunge katikati ya mji wa London, kulikuwa na watu wengi licha ya wito wa serikali kutokongamana kwa hofu ya kusambaa kwa virusi vya corona.

Nchini Australia , kulikuwa na maandamano makubwa katika miji ya Sidney na Melbourne na Brisbane yalioangazia jinsi raia wenye chimbuko la Australia walivyokuwa wakinyanyaswa. Pia kulikuwa na maandamano nchini Ufaransa, Ujerumani na Uhispania.


EmoticonEmoticon