Mahakama Yaamua Rais Mteule Wa Burundi Kuapishwa Mara Moja

Evariste Ndayishimiye
Mahakama ya kikatiba ya Burundi imeamua kuwa rais mteule Meja Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye aapishwe urais mara moja na hakutakuwa na rais wa mpito.
Toka kutangazwa kifo cha Nkurunziza mapema wiki hii kumekuwa na ombwe la uongozi nchini humo.
Katiba ya nchi hiyo inaeleza kuwa spika wa bunge atatakiwa kuchukua nafasi hiyo kwa mpito pale rais anapofariki. Hata hivyo Spika Pascal Nyabenda hakuapishwa mara moja hali ambayo wachambuzi wametafsiri kama ishara ya msuguano ndani ya chama tawala nchini humo.
Baraza la mawaziri nchini Burundi katika kikao chake cha Alhamisi liliamua kulipeleka suala hilo katika mahakama ya katiba na kutangaza litaongoza nchi kwa pamoja hadi rais mpya atakapoapishwa.
Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano uliokuwa chini ya uongozi wa Makamu wa Rais wa kwanza Gaston Sindimwo.
Chama cha mawakili nchini Burundi kimetoa wito wa kuapishwa mara moja kwa rais mteule.
Wakati mahakama ikitoa uamuzi huo, taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema Rais Mteule Ndayishimiye, pia ni mgonjwa.
Mke wake alipigwa picha akitia saini kitabu cha maombolezo japo Ndayishimiye hajaonekana hadharani.
Ndayishimiye wa chama tawala cha CNDD-FDD aliyechaguliwa Mei 20 awali ilikuwa aapishwe mwezi Agosti.


EmoticonEmoticon