Mshirika Mkuu Wa Serikali Ya Rais Felix Tshisekedi Nchini DR Congo Amehukumiwa Kifungo Cha Miaka 20 Jela

Vital Kamerhe
Mshirika mkuu wa serikali ya rais Felix Tshisekedi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Vital Kamerhe amehukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa ufisadi na wizi wa takriban dola milioni 50 za Marekani.
Kamerhe ni mwanasiasa maarufu katika siasa za taifa la DR Congo na ndie mtu muhimu wa muungano uliomsaidia rais Felix Tshisekedi kuchukua madaraka.
Ndie mwansiasa mkuu zaidi kukabiliwa na mashtaka katika taifa la Dr Congo ambapo kuna ufisadi wa kiwango cha juu.
''Katika kila tulichosikia, mahakama imebaini ukweli kuhusu makosa ya wizi wa dola milioni 48, 831, 183 za Marekani'', alisema jaji Pierrot Bankenge Mvita katika uamuzi wake.
Wakati jaji alipokuwa akitangaza hukumu hiyo , Vital Kamerhe alisalia mtulivu na hata kutabasamu mara kwa mara.
Hatoruhusiwa kuwania wadhifa wowote kwa miaka 10 baada ya kuhudumia hukumu yake na hata kushikilia wadhfa wowote wa serikali.
Mahakama vilevile itapiga tanji akaunti zake zote za benki pamoja na zile za ndugu zake , mbali na mali ilionunuliwa na fedha zilizoibwa.
Kamerhe amekana kuiba fedha zilizotengewa mradi wa ujenzi wa nyumba za serikali chini ya uogozi wa rais Tshisekedi na kuyataja mashtaka hayo kuwa ya kisiasa. Wakili wake Jean Marie Kabengela Ilunga aliutaja uamuzi huo kama ukiukaji wa haki za kibinadamu na kusema kwamba atakata rufaa .


EmoticonEmoticon