Rais wa Kenya Akataa Kufuta Uwezekano Wa Kuwa Waziri Mkuu

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amekataa kufutilia mbali uwezekano kwamba wadhfa wa waziri mkuu huenda ukabuniwa katika kura ya maoni ijayo kama njia ya kumfanya kuwa na madaraka hata baada ya muda wake wa kikatiba wa mihula miwili kama rais kukamilika.
Bwana Kenyatta anaachilia madaraka 2022. Katika mahojiano na gazeti la Financial Times, rais Uhuru alikataa kuzungumzia kuhusu 'nyadhfa za kisiasa ambazo hazipo'.
Hatahivyo alisema waziwazi kwamba hatosalia kuwa rais baada ya kukamilika kwa mihula yake miwili, akisema kwamba katiba na watu wa Kenya wako wazi kuhusu suala hilo.
''Wakenya wanaelewa kuhusu mihula miwili ya urais tangu 2002, wakati ilipoanza kutekelezwa . Hakuna rais hata mmoja aliyevunja sheria hiyo . Na sina nia kuwa rais wa kwanza kufanya hivyo'', alisema.
Rais amesema kwamba Kenya itaandaa kura ya maoni hivi karibuni, kulingana na yeye ili kubadilisha baadhi ya vifungu vya katiba ukweli ambao pia walioitengeneza wanakubaliana nao.
Pia alizungumzia wasiwasi kuhusu biashara huru inayojadiliwa kati ya Kenya na Marekani , akisema yatakuwa majadiliano ya usawa licha ya tofauti ya kiuchumi na kisiasa ya mataifa hayo mawili.
Mashirika mengi ya wanaharakati , ambayo yanadai kwamba makubaliano hayo ya kibiashara yatakuwa mabaya kwa uchumi wa Kenya , yalituma ujumbe wa kupinga chini ya alama ya reli #NoToKenyaUSFTA.
Bwana Kenyatta pia alikuwa na ujumbe kwa wale wanaoshiriki katika maandamano ya Black Lives Matter nchini Marekani na duniani kwa jumla : All Lives Matter , lakini hakufai kuwa na ukandamizaji wa kundi lolote katika jamii''.


EmoticonEmoticon