WhatsApp Yazindua Huduma Ya Kutuma Na Kupokea Pesa

Malipo ya Whatsapp
WhatsApp imezindua huduma ya malipo ya kidijitali nchini Brazil katika juhudi za kutumia umaarufu wake kuingia kwenye masoko yanayoibuka katika ulimwengu wa biashara.
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo Facebook ambayo ni mmiliki wa WhatsApp inapania kujikita zaidi kwenye biashara za kidijitali ambazo zitajumuisha mitandao yake yote.
Huduma hiyo inayofahamika kama WhatsApp Pay itawawezesha watumiaji wa mtandao huo kutumiana pesa bila malipo au kununua bidhaa kutoka kwa wafanyibiashara wadogo.
Mwezi Januari, afisa mkuu mtendaji wa Mark Zuckerberg alielezea mpango wa kampuni hiyo kutoa huduma zake India, Indonesia na Mexico.
Katika blogu yake WhatsApp, aliangazia huduma hiyo ikisema uzinduzi wake ni sehemu ya mpango mkubwa wa kuimarisha malipo ya kidijitali kupitia mitandao yote inayomilikiwa na Facebook.
"Kwa sababu huduma ya malipo kupitia WhatsApp inawezeshwa na Facebook Pay, siku zijazo tunataka kuwawezesha watu binafsi na wafanyabiashara kutumia mfumo mmoja wa malipo wakiwa katika programu tumishi ama app za Facebook."
Japo huduma ya malipo kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine haitatozwa ada yoyote wafanyibiashara wadogo watatozwa ada ya "kuwawezesha kupokea malipo kutoka kwa wateja wao," blogu hiyo iliandika.
WhatsApp ina jumla ya watumiaji 120 milioni nchini Brazil, hali inayofanya taifa hilo kuwa soko lake la pili kwa ukubwa baada ya India.
Kampuni hiyo tayari imeanza kufanyia majaribio huduma hiyo ya malipo India, ambako ina watumiaji 400 milioni.
Hata hivyo, juhudi za kampuni hiyo kuzindua huduma ya WhatsApp Pay nchini India imesitishwa kwa miaka miwili kutokana na masuala ya kisheria.


EmoticonEmoticon