Raisi Wa Marekani Akiri Janga La Corona Litaathiri Vibaya

Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa mwenendo wa ugonjwa wa corona nchini humo huenda ukawa "mbaya zaidi kabla ya hali kuimarika", wakati alipofufua tena mkutano wake na wanahabari.
Bw. Trump pia ametoa wito kwa Wamarekani wote kuvalia barakoa, akisema kuwa "zitasaidia kudhibiti maambukizi" na kwamba ni ishara ya "uzalendo".
Rais, hakua amevalia barakoa wakati akitoa maelezo kwa wanahabari, lakini aliwahi kupuuza suala la kuvaa kifaa kinga hicho.
Inasemekana wasaidizi wake wamemuasa kuchukua hatua zenye malengo wakati ambapo maambukizi yanazidi kuongezeka kote Marekani.
Utoaji taarifa kuhusu corona kwa vyombo vya habari kutoka Ikulu ya Marekani, mwisho ilikuwa Aprili punde tu baada ya Trump kusema kuwa virusi hivyo vinaweza kutibiwa kwa watu kujipaka dawa za kuua vijidudu.
Baada ya miezi kadhaa, taarifa yake ya Jumanne ambayo ilionekana kupangwa, rais aliashiria kuunga mkono kile ambacho maafisa wa afya wamekuwa wakisema kupitia jopo lake la kukabiliana na ugonjwa huo na kuonya kwamba: "Kwa bahati mbaya hali huenda ikawa mbaya zaidi kabla ya kuanza kubadilika.
"Wakati mwingine huenda sipendi kusema kuhusu mambo, lakini hivyo ndivyo ilivyo."
Aliongeza: "Tunataka kila mmoja ikiwa atashindwa kutekeleza kanuni ya kutokaribiana, avae barakoa.
"Ama uwe unapenda barakoa au la, zina machango wake, zitakuwa na athari yake na tunahitaji kila kitu tunachoweza kupata."
Bwana Trump - ambaye zaidi ya mara moja alirejelea kuwa ugonjwa wa Covid-19 ni "virusi vya China" - akiwa anatoa taarifa hiyo, alitoa barakoa mfukoni kwake, lakini hakuivaa.
Rais huyo ana kibarua kigumu wakati anapotafuta kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi wa urais Novemba dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Democratic, Joe Biden, kulingana na kura za maoni.
Bwana Biden Jumanne alimshutumu Bwana Trump kwa kushindwa kukabiliana na janga la virusi vya corona. "Amewaondokea nyinyi, ametenga nchi hii," aliyekuwa makamu rais wa Marekani alisema.


EmoticonEmoticon