Umoja Wa Ulaya Hatimaye Wakubaliana Kuufufua Uchumi Wao

Umoja wa Ulaya
Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya hatimaye Jumanne asubuhi walifikia makubaliano ya yuro bilioni 750 za kuufufua uchumi wao. 

Pesa hizi ni za kukabiliana na athari zilizotokana na janga la virusi vya corona.

Viongozi hao walioonekana wenye uchovu wamekubaliana bajeti ya yuro trilioni 1.82 pia pamoja na hizo pesa za kufufua uchumi baada ya janga la virusi vya corona. 

Hatua hii imefikiwa kufuatia majadiliano ya siku nne ya usiku na mchana yaliyojawa na makabiliano na ubishi mkali kuhusiana na pesa na nguvu katika mojawapa ya mkutano wao mrefu zaidi wa kilele kuwahi kushuhudiwa.

Hizo bilioni 750 zitatolewa kama mkopo kwa nchi zilizoathirika vibaya zaidi na janga hilo huku makubaliano yakiafikiwa pia kuhusiana na bajeti hiyo ya miaka saba ya zaidi ya trilioni moja.

Charles Michel ni mwenyekiti wa mkutano huo wa kilele.
"Tumeonyesha imani kwa mustakabali wetu na makubaliano haya yanaonyesha kuwa Ulaya ni nguvu ya vitendo. Tumejadiliana kuhusu pesa ila makubaliano haya ni zaidi ya pesa. 
Naamini kwamba makubaliano haya yataonekana kama sehemu muhimu ya safari ya Ulaya," alisema Michel.
Mkutano huo wa kilele ulikuwa umepangiwa kufanyika kwa kipindi cha siku mbili ila kulilazimika kuongezwa siku mbili zengine kutokana na tofauti zilizokuwa baina ya viongozi wa nchi ishirini na saba za umoja huo.


EmoticonEmoticon