Wabunge Marekani Waamriwa Kuvaa Barakoa

Nancy Pelosi
Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi ameamuru kuwa wabunge na wafanyakzi wote wa chombo hicho watapaswa kuvaa barakoa katika kipindi chote cha janga la virusi vya corona.

Akizungumza bungeni jana Jumatano, spika Pelosi amesema anatumai wabunge na wafanyakazi wote wataheshimu sharti hilo kama ishara ya kulinda afya na usalama wa kila mmoja ndani ya majengo ya Bunge.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya mbunge wa chama cha Republican Louie Gohmert aliyepinga vikali uvaaji barakoa kutangaza kuwa ameambukizwa virusi vya corona jana Jumatano.

Kulingana na Pelosi, chini ya kanuni hiyo mpya wabunge wataruhusiwa tu kuondoa barakoa wakati wa kuhutubia au kutoa michango mbele ya Bunge.

Hayo yanajiri wakati Marekani imefikisha idadi ya vifo 150,000 vya COVID-19 ambayo ni kubwa kuliko taifa lingine lolote duniani.


EmoticonEmoticon