Chapisho Baya Dhidi Ya Mtume Muhammad Lapelekea Watu Watatu Kufariki

Watu watatu wamefariki katika mji wa Bangalore nchini India baada ya maafisa wa polisi kuwafyatulia risasi waandamanji waliokuwa wakiandamana dhidi ya chapisho la kufuru katika mtandao wa facebook.

Makundi ya watu yalikusanyika nje ya nyumba ya mwanasiasa mmoja ambaye ndugu yake alituhumiwa kuchapisha chapisho baya dhidi ya mtume Muhammad.

Walichoma moto magari na kumshambulia afisa wa polisi aliewasili katika eneo la tukio akiwa amebeba mawe, polisi waliambia BBC Hindi.

Polisi wamemkamata mtu huyo na wengine 110 waliokuwa katika mkusanyiko huo.

Kamishna wa mji huo Kamal Pant alisema kwamba takriban maafisa 60 wa polisi akiwemo afisa mmoja mkuu walijeruhiwa katika ghasia hizo siku ya Jumanne usiku.

Masharti ya kutotoka nje yaliwekwa katika wilaya mbili za eneo hilo, alisema.

Wakati huohuo maafisa wa polisi walituma ujumbe wa twitter kwamba hali imedhibitiwa, wakiongeza kwamba polisi walifyatua risasi kuwatawanya waandamanaji baada ya kutumia vitoa machozi.

Vifo hivyo vilithibitishwa na waziri wa jimbo la Karnataka ambapo Bangalore ndio mji mkuu.

Ghasia hizo zilianza baada ya waandamanaji kupiga kambi nje ya nyumba hiyo ya mwanasiasa mbali na kituo kimoja cha polisi baada ya kuliona chapisho hilo, ambalo vyombo vya habari vinasema limefutwa.


EmoticonEmoticon