Japan Yakumbuka Miaka 75 Ya Bomu La Atomiki Hiroshima

Japan imefanya kumbukumbu ya miaka 75 tangu kuangushwa kwa bomu la kwanza la atomiki kwenye mji wa Hiroshima, huku meya wa mji huo akiitaka jumuiya ya kimataifa kuukataa ule aliouita uzalendo uliojengwa kwenye ubinafsi.

Hakukuwa na mkusanyiko wa maelfu ya watu kwenye Bustani ya Amani katikati ya mji wa Hiroshima kama inavyokuwa kwenye miaka mingine. Janga la virusi vya korona vilivyosambaa kote duniani limezifanya kumbukumbu za mwaka huu kukosa mahudhurio yake ya kawaida.

Watu pekee walioruhusiwa kuhudhuria kumbukumbu hizo ni manusura wa mashambulizi hayo yaliyofanywa na Marekani pamoja na familia zao. 

Majira ya saa mbili na robo asubuhi ya tarehe 6 Agosti 1945, ndege ya kijeshi ya Marekani chapa B-29 Enola Gay iliangusha bomu lililopewa jina la "Mvulana Mdogo" na kuwauwa hapo hapo watu 140,000 kati ya wakaazi 350,000 wa mji huo.

Maelfu ya wengine walikufa siku za baadaye kutokana na majeraha na mionzi ya atomiki. Alkhamis ya leo, katika muda huo huo bomu hilo liliporipuka, watu walisimama na kunyamaza kimya kwa muda kuwakumbuka wahanga hao. 

Meya Kazumi Matsui wa Hiroshima alisema kwamba ni kuzuka kwa hisia kali za utaifa ndiko kulikopelekea Vita vya Pili vya Dunia na mabomu ya atomiki, jambo ambalo halipaswi tena kuachwa likarejea.

"Jamii iliyostaarabika inapaswa kuukataa uzalendo uliojikita kwenye ubinafsi na uungane dhidi ya vitisho vyote," alisema meya huyo.


EmoticonEmoticon