Maafisa Wa Bandari Wakiwekwa Katika Kifungo Cha Nyumbani Lebanon

Baadhi ya maafisa wa mji wa Beirut wamewekwa katika kifungo cha nyumbani huku wakisubiri uchunguzi kuhusu mlipuko mkubwa wa siku ya Jumanne, kulingana na serikali ya Lebanon.

Mlipuko huo uliwaua watu 135 na kuwajeruhi wengine 4000. Hali ya tahadhari ya wiki mbili imeanza kutekelezwa nchini humo.

Rais Michel Aoun alisema kwamba mlipuko huo ulisababishwa na tani 2750 za Amonium Nitrate iliokuwa imehifadhiwa katika ghala moja katika bandari ya mji huo.

Afisa mkuu wa masuala ya forodha Badri Daher alisema kwamba shirika lake lilitoa wito kwa kemikali hiyo kuondolewa, lakini hilo halikufanyika.

''Tumewaachia wataalamu kufichua sababu zake'', alisema. Amonium Nitrate hutumika kama mbolea katika kilimo na pia kama kilipuzi.

Katika kikao cha dharura cha baraza la mawaziri siku ya Jumatano, rais Aoun alisema: Hakuna maneno yanaweza kuelezea tishio ambalo limekumba Beirut usiku uliopita, na kuufanya mji huu kama uliokumbwa na janga.

Wataalamu katika chuo kikuu cha Sheffield nchini Uingereza wanakadiria kwamba mlipuko huo ulikuwa na kiwango cha 1/10 cha nguvu za bomu la nyuklia lililoangushwa katika mji wa Japan wa Hiroshima wakati wa vita vya pili vya dunia na limetajwa kuwa mlipuko mkubwa wa bomu lisilo la nyuklia katika historia .


EmoticonEmoticon