Mwanamuzi Wa Nigeria Amehukumiwa Kifo Kwa Kukufuru

Mwanamuzi nchini katika jimbo la kaskazini mwa Nigeria la Kano amehukumiwa kifo kwa kunyongwa kwa kumkufuru Mtume Mohammad

Mahakama ya juu ya kiislamu inayotumia Sharia katika eneo la Hausawa Filin Hockey katika jimbo la Kano imesema kuwa Yahaya Sharif-Aminu, mwenye umri wa miaka 22, alipatikana na hatia ya kukufuru kwa wimbo wake uliosambazwa kupitia mtandao wa WhatsApp mwezi Machi. Bwana Sharif-Aminu hakukanusha mashitaka.

Jaji Khadi Aliyu Muhammad Kani alisema kuwa anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo dhidi yake.

Majimbo ya kaskazini mwa Nigeria yanayokaliwa na Waislamu wengi hutumia sheria ya kiislamu na sheria ya kawaida, ambayo haitumiwi kwa watu ambao sio wafuasi wa dini ya kiislamu.

Ni moja tu ya hukumu za kifo iliyopitishwa na mahakama za sharia nchini Nigeria tangu zilipoanzishwa mwaka 1999.

Mwanamuzi huyo ambaye kwa sasa anashikiliwa mahabusu, alikua amejificha baada ya kutunga wimbo huo.

Waandamanaji walikua wamechoma moto nyumba ya familia yake na kukusanyika nje ya makao makuu ya polisi ya kiislamu huku Hisbah, wakidai hatua ichukuliwe dhidi yake.

Wakosoaji wanasema wimbo ulikufuru kwani ulimsifu imam kutoka Waislam wa Tijaniya kiasi kwamba ulimpatia hadhi ya juu kuliko Mtume Muhammad.

'Hukumu itakua mfano kwa wengine '

Kiongozi wa maandamano ambayo yalidai kukamatwa kwa mwanamuziki huyo mwezi Machi, Idris Ibrahim, aliiambia BBC kuwa hukumu itakuwa kama onyo kwa wengine "wanaojaribu kufuata nyayo za Yahaya"."Niliposikia kuhusu hukumu nilifurahi sanakwasababu inaonesha kuwa maandamano yetu hayakua ya bure.

"Hukumu hii itakua ni mfano kwa wale ambao wanahisi kuwa wanaweza kutukana dini yetu au mtume na waendelee kuwa huru," alisema.


EmoticonEmoticon