Raisi Wa Urusi Asema Chanjo Ya Corona Imeidhinishwa Tayari Kwa Matumizi

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kwamba chanjo iliyotengenezwa ndani ya Urusi kwa ajili ya ugonjwa wa Covid-19 imeidhinishwa kwa matumizi baada ya kufanyiwa majaribio kwa binadamu chini ya miezi miwili.

Bwana Putin amesema kwamba chanjo hiyo imepita vigezo vyote vilivyowekwa na kuongeza kwamba binti yake tayari amepatiwa.

Maafisa wamesema kuwa wanampango wa kuanza kutoa chanjo hiyo kwa umma kuanzia Oktoba.

Wataalamu wameonesha wasiwasi wao kuhusu kasi ya kazi ya Urusi na kusema kuwa watafiti huenda wametumia njia za mkato.

Huku wasiwasi ukiendelea kuhusu uwezekano wa usalama kuingiliwa wiki iliyopita Shirika la Afya Duniani (WHO) liliitaka Urusi kufuata miongozo ya kimataifa ya kutengeneza chanjo dhidi ya virusi vya corona.

Chanjo iliyotengenzwa na Urusi sio miongoni mwa orodha ya zile za WHO ambazo zimefika awamu ya tatu ya majaribio kunakohusisha majaribio kwa watu wengi zaidi.

Akiitaja chanjo hiyo kuwa ya kwanza Duniani, Rais Putin amesema chanjo iliyotengenezwa na taasisi ya Moscow ya Gamaleya, inatoa "kinga endelevu" dhidi ya virusi vya corona.

Waziri wa Afya Mikhail Murashko amesema chanjo hiyo imethibitisha kuwa salama na yenye ufanisi", na kupongeza kwamba ni hatua kubwa kuelekea ushindi kwa mwanadamu dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.

Wiki iliyopita, Serikali ya Urusi ilitangaza kwamba inajitayarisha kuanza kutoa chanjo hiyo kwa umma baada ya majaribio yake kufanikiwa.

Credit:Bbc


EmoticonEmoticon