Serikali Ya Lebanon Yatangaza Hali Ya Hatari, Jeshi Lapewa Madaraka

Serikali ya Lebanon imetangaza wiki mbili za hali ya hatari, ambapo jeshi limepewa madaraka kamili, katika wakati huu uchunguzi ukiendelea, kufuatia mripuko mkubwa kwenye bandari ya Beirut uliouwa hadi sasa watu 135. 

Kwenye hotuba yake kwa taifa hapo jana, Rais Michel Aoun alisema msiba huo hauna maelezo. Waziri Mkuu Hassan Diab ametangaza pia siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia leo. 

Uchunguzi wa awali unaonesha kwamba uzembe ndio uliosababisha mripuko huo jioni ya Jumanne. Zaidi ya watu 5,000 wamejeruhiwa na makumi ya wengine hawajulikani walipo hadi sasa. 

Maafisa wanasema watu robo milioni wamejikuta wakiwa hawana nyumba zinazofaa kukaliwa, baada ya mtikisiko wa mripuko huo kuharibu majengo na vifaa vyao vya ndani. 

Timu za waokowaji zimeendelea kufukuwa vifusi kuwasaka manusura, huku idadi ya waliokufa kwenye mkasa huo wa aina yake ikitazamiwa kupanda.


EmoticonEmoticon