Bahrain, UAE Zaweka Mahusiano Ya Kidiplomasia Na Israel, Trump Aongoza Sherehe Hizo

Rais wa Marekani Donald Trump ameongoza sherehe ya kuwekeana uhusiano wa kibalozi kati ya Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain, akiimarisha nafasi ya kuchaguliwa tena mwezi Novemba. 

Akizungumza wakati wa kuyasaini makubaliano hayo katika Ikulu ya White House mjini Washington, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameisifu hatua hiyo, akisema inaweza kuwa mwanzo wa kumaliza kabisa uhasama wa muda mrefu kati ya nchi yake na ulimwengu wa kiarabu.

Amesema ilikuwa siku ya kihistoria inayoashiria mapambazuko mapya ya amani, na kusema hatua ya amani waliyopiga leo, itadumu. Netanyahu ameelezea matumaini yake, kuwa mfano wa Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu utafuatwa na nchi nyingine za kiarabu.

Waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abdullah bin Zayed al-Nahyan, binafsi amemsifu Netanyahu, ambaye amesema amechagua amani kwa kusitisha unyakuaji wa ardhi za Wapalestina. 

Rais Donald Trump ambaye kusainiwa kwa makubaliano haya ni muhimu kwa sera yake ya nchi za nje huku akielekea katika uchaguzi wa mwezi Novemba, amesema historia ya Mashariki ya Kati imebadilisha mkondo.

''Baada ya miongo ya mgawanyiko na mizozo, tunafikia mapambazuko mapya kwa Mashariki ya Kati. Shukrani kwa viongozi jasiri wa nchi hizi tatu, tunapiga hatua kubwa kuelekea mustakabali ambapo watu wa dini na asili tofauti wataishi pamoja kwa amani na ustawi.'' Amesema Trump.


EmoticonEmoticon