Jeshi La Mali Kuunda Serikali Ya Mpito Ya Miezi 18

Jeshi la mapinduzi nchini Mali limeapa kuunda serikali ya mpito ya muda wa miezi 18 ili kuirejesha nchi hiyo katika utawala wa kiraia baada ya mapinduzi ya mwezi uliopita dhidi ya serikali ya rais Ibrahim Boubacar Keita

Kamati iliyoteuliwa na jeshi hilo la mapinduzi iliidhinisha kwa kauli moja ''mkataba wa mpito'' katika mkutano wa faragha kuhusu ubadilishanaji wa mamlaka hatua inayotoa njia kwa serikali ya muda itakayoongoza kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mpya.

Lakini moja ya masuala tata zaidi bado halijapata ufumbuzi kuhusu iwapo serikali hiyo ya mpito itaongozwa na raia ama mwanajeshi. Moussa Camara, katibu wa kamati hiyo, amesema jana kwamba serikali mpya itaundwa na wanachama zaidi ya 25, pamoja na waziri mkuu. 

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa chini ya mkataba wa awali, rais wala mawaziri wa serikali ya mpito hawawezi kuwania madaraka muda wao wa kuhudumu utakapokamilika.
    
Camara amesema mashauriano ya siku tatu na viongozi wa kisiasa na makundi ya kiraia yaliunda mkataba wa mpito ambao pia utajumuisha makamu wa rais na baraza la mpito ambalo litahudumu kama bunge la taifa. 

Rais na Makamu wa rais watachaguliwa na kundi la watu watakaoteuliwa na uongozi wa jeshi.


EmoticonEmoticon