Kim Kardashian Ajiunga na Mgomo Dhidi ya Mitandao ya Kijamii

Mtangazaji na mfanyabiashara maarufu duniani, Kim Kardashian West, na wasanii wengine wametangaza kufunga akaunti zao za mitandao ya kijamii kupinga kuenea kwa chuki, propaganda na taarifa zisizo sahihi.

“Taarifa potofu zinazowekwa mitandaoni zina athari kubwa,” Kardashian  aliandika.

Hatua hiyo ni sehemu ya kampeni ya kupinga chuki ifahamikayo kama #StopHateforProfit ambayo imeandaliwa na wanaharakati wa haki za raia. Wasanii hao watafunga akaunti zao za mitandao ya kijamii kwa muda 24 , siku ya Jumatano.

“Siwezi kukaa kimya wakati mitandao ikiendelea kuridhia kusambazwa kwa habari za chuki, propaganda na taarifa zisizo sahihi — zilizoandaliwa na makundi yanayotaka kuigawa Marekani, alisema,”  aliongeza.

“Upotoshaji wa taarifa unaotumwa mitandaoni una athari kubwa katika uchaguzi na kuminya demokrasia yetu,” aliongeza.

Wasanii wengine ambao wamekubali kushiriki katika zoezi hilo ni pamoja na waigizaji Leonardo DiCaprio, Sacha Baron Cohen na Jennifer Lawrence, na muimbaji Katy Perry.

“Siwezi kukaa tu bila kufanya kitu wakati mitandao ya kijamii inafumbia macho makundi ya watu wanaotuma ujumbe na maoni ya chuki na yasiyo na ukweli wowote,” Perry aliandika katika mtandao wa Instagram.

Muigizaji Ashton Kutcher, ambaye ana mamilioni ya wafuasi pia amejiunga katika kampeni hiyo na alisema, “mitandao hii haikutengenezwa ili kusambaza chuki na ghasia”.

Waandaaji wa kampeni ya #StopHateforProfit, ambayo ilizinduliwa Juni, imeishutumu Facebook na Instagram kwa kushindwa kusitisha taarifa za chuki na za upotoshaji.

Kundi hilo limewalenga Facebook, ambayo pia inamiliki Instagram na WhatsApp na mwaka jana kampuni hiyo iliweza kupata kodi ya matangazo ya karibu dola bilioni sabini $70bn (£56.7bn). 

Maelfu ya biashara na makundi ya kutetea haki za raia yalisaini kampeni hiyo.

“Tunakaribia kufikia uchaguzi mmoja ambao ni muhimu sana katika historia ya Marekani,” kundi hilo liliandika katika taarifa yake.


EmoticonEmoticon