Mfalme Wa Saudi Arabia Amwambia Trump Suala La Palestina Litatuliwe Kwa Haki

Mfalme wa Saudi Arabia Salman amemwambia rais Donald Trump wa Marekani  katika mazungumzo ya  simu jana kuwa taifa hilo  la kifalme lina nia  ya  kufikiwa  suluhisho la haki na la  kudumu  katika suala  la  Palestina. 

Mfalme Salman alisema  hilo  ni sehemu kuu  ya kuanzia ya juhudi  za  pendekezo  la amani  la mataifa  za  Kiarabu. 

Viongozi  hao walizungumza kwa simu kufuatia  makubaliano ya kihistoria  yaliyosimamiwa na  Marekani  mwezi uliopita ambayo Umoja  wa Falme za Kiarabu  ulikubali  kuwa  taifa  la  tatu  la Kiarabu  kurejesha  uhusiano  wa kawaida  na  Israel baada  ya Misri na  Jordan.

Mfalme Salman  alimwambia  Trump anakubaliana  na  juhudi za Marekani  za  kuunga  mkono  amani  na  kwamba  Saudi Arabia inataka  kuona  suluhisho la kudumu  na  la  haki  katika  suala  hili  la Palestina chini  ya  juhudi  za  amani  za  mataifa  ya  Kiarabu zilizopendekezwa  na  taifa  hilo  mwaka  2002.

Chini  ya pendekezo  hilo, mataifa  ya  Kiarabu  yamependekeza kwa Israel  kurejesha  uhusiano wa  kawaida  ili kuweza kufikiwa makubaliano ya kupatiwa  Wapalestina taifa lao  na Israel kujitoa kabisa  kutoka  katika  ardhi za mataifa  ya  Kiarabu ilizoziteka  katika vita vya mwaka 1967 vya mashariki  ya  kati.


EmoticonEmoticon