Shinikizo Lazidi Kwa Raisi Wa Kenya Uhuru Kuhutubia Bunge

Shinikizo zimeendelea kutolewa kwa rais Uhuru Kenyatta kuhutubia bunge.

Rais awali alikuwa ametoa hotuba zake bungeni mwezi Machi na Mei. Hata hivyo kutokana na janga la corona rais bado hajatoa hotuba yake.

Kulingana na kanuni za bunge la kitaifa ni kwamba rais atahutubia taifa angalau mara moja kila mwaka.
Kipengele cha 132 cha katiba kinamtaka rais kuhutubia kikao cha pamoja cha bunge kuzungumzia masuala yanayoathiri taifa.

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’a siku ya Jumatano alisema kwamba rais Uhuru Kenyatta anahitajika haraka iwezekanavyo kuhutubia taifa kuhusu hali ya uchumi wa taifa.

Mwandani huyo wa naibu rais William Ruto anataka rais Kenyatta kueleza mikakati ya serikali kukwamua uchumi wa taifa.

Ichung’wa alisema ni vyema kwa wananchi kujua mipango ya serikali kuendeleza miradi ya maendeleo baada ya athari za janga la Covid-19.

Alisema hotuba hiyo ya rais itawezesha wakenya kufahamu vile serikali inapanga kushugulikia changamoto wanazopitia wakenya kutokana na janga la Covid-19.

“Tuna hamu kusikiza yale rais amepanga kuhusiana na ajenda yake ya kuhakikisha kwamba maendeleo na mikakati ya kupiga jeki uchumi wa taifa inarejelewa baada ya janga la corona,” mbunge huyo alisema.

Alisema hakuna sababu ya ‘ikulu ya rais kushindwa kupanga hotuba ya rais kwa bunge kuzungumzia ufufuzi wa uchumi.
Ichung’wa alipendekeza kuwekwa kwa hema kubwa katika uwanja wa KICC, majengo ya bunge, Bomas au Kasarani ikiwa wabunge hawataweza kutoshea bungeni kwa rais kutoa hotuba yake.

Amesema ufichuzi kwamba takriban wakenya milioni 1.6 wamepoteza kazi ni sababu tosha kwa rais kuandaa mkutano huo haraka iwezekanavyo.
Credit:Radiojambo


EmoticonEmoticon