UN: Mataifa Yatekeleze Vikwazo Kuhusu Libya

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalotaka nchi zote kuzingatia utekelezaji wa vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa vilivyowekwa dhidi ya Libya. 

Azimio la Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipitishwa siku ya Jumanne ambapo pia limezitaka nchi zote kuondowa mamluki wao walioko ndani ya nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pia limetowa mwito wa kufanyika mazungumzo ya kisiasa na kusitishwa mapigano katika nchi hiyo inayokabiliwa na vita vikubwa,huku likibaini kwa msisitizo kwamba hakuna suluhisho la kijeshi katika mgogoro huo.

Katika mchakato wa kulipigia kura azimio hilo kuhusu Libya wanachama 13 waliunga mkono na kuliidhinisha huku Urusi na China zikijizuia kupiga kura.

Kwa hivi sasa Libya toka kipindi cha miaka kadhaa baada ya kuangushwa madarakani na kuuwawa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Muammar Ghaddafi, imetumbukia zaidi kwenye mgogoro na machafuko na imegawika vipande viwili, Mashariki na Magharibi, ambapo kila upande unaungwa mkono na makundi ya wapiganaji na wanamgambo wanaosaidiwa na nchi mbali mbali za kigeni zenye nguvu.


EmoticonEmoticon