Armenia, Azerbaijan Zalaumiana Kukiuka Makubaliano Ya Amani

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezitolea wito Armenia na Azerbaijan kuheshimu makubaliano mapya ya kusitisha mapigano na kulaani mashambulio dhidi ya raia wakiwa wanazozania eneo la Nagorno-Karabakh.

Guterres amelaani hasa shambulio la kombora lilopiga eneo la makazi la mji wa Ganja wa Azerbaijan siku ya Jumamosi, na kuua watu 13 wakiwemo watoto.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa katibu mkuu huyo, Stephane Dujarric, Guterres amesema amesikitishwa na ripoti za hivi karibuni za raia waliopoteza maisha ikiwa ni pamoja na watoto katika mji wa Ganja, na kukitaja kuwa ni kitendo kisichokubalika.

Aidha Guterres amesema anatarajia pande zote mbili kutii ahadi hiyo ya kusitisha mapigano ya Oktoba 18, na kuanza tena mazungumzo bila kuchelewa.

Armenia na Azerbaijan zilikubaliana kusitisha mapigani Jumamosi kutoka saa sita usiku, lakini kila mmoja alimlaumu mwenzake kwa kukiuka makubaliano hayo jana Jumapili.

Hilo ni jaribio la pili la kutaka kusitisha mapigano tangu mzozo huo kuzuka Nagorno-Karabakh mnamo Septemba 27. Mapigano hayo yamesababisha mamia ya vifo vya wanajeshi na raia wa kawaida.

Kulingana na maafisa wa Nagorno-Karabakh, wanajeshi wao 673 wameuawa katika mapigano hayo mapya. Azerbaijan kwa upande wake haijaweka wazi idadi ya vifo vya wanajeshi wake, lakini imesema raia 60 wamekufa hadi sasa na 270 wamejeruhiwa.


EmoticonEmoticon