Baadhi Ya Wafungwa Waliotoroka DRC Warudi Wenyewe Gerezani

 

Wafungwa waliorudi wamewaambia maafisa kwamba walilazimishwa kutoroka na wanapendelea kuendelea kukaa gerezani badala ya kuishi na waasi. 

Wafungwa 20 kati ya 1,300 waliotoroka gerezani katika mji wa Beni, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wamerudi gerezani muda mfupi baada ya kutoroka.

Wafungwa waliorudi wamewaambia maafisa kwamba wanapendelea kuendelea kukaa gerezani badala ya kuishi na waasi.

Kulingana na Meya wa mji wa Beni Modeste Bakwanamaha, wafungwa waliorudi wamesema kwamba “walichukuliwa kwa nguvu na kwamba wamewatoroka waasi wa Allied Democratic Forces –ADF - waliowateka nyara baada ya kuvunja gereza jumanne asubuhi.”

Watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki, wanaoaminika kuwa wapiganaji wa kundi la ADF walivamia gereza la Kangbayi, mjini Beni na kuachilia huru zaidi ya wafungwa 1,300. Wafungwa 100 pekee walisalia gerezani.

Kulingana na Meya Bakwanamaha, “washambuliaji walikuwa wengi na walifanikiwa kuvunja milango ya gereza kwa kutumia machine za wahunzi zinazotumia umeme.”


EmoticonEmoticon