Rais wa
benki ya dunia, David Malpass, amesema baadhi ya wakopeshaji kutoka
nchi zilizoendelea kiuchumi maarufu kama G20, bado wanasita kurefusha kwa mwaka
mmoja, kipindi cha kusamehe madeni kwa nchi maskini zilizoathiriwa na janga la
virusi vya corona.
Kiongozi huyo wa benki ya
dunia amesema huenda wiki hii wakopeshaji hao wakaafikiana kuzisamehe nchi
maskini kulipa madeni kwa kipindi cha miezi sita.
Akizungumza na waandishi
wa habari, Malpass, amesema wakopeshaji wa G20 hawajafikia makubaliano kuhusu
pendekezo la benki ya dunia na shirika la kimataifa la fedha IMF, la kurefusha
kipindi cha mwaka mmoja kwa mataifa masikini yaweze kulipa madeni yao.
Mawaziri wa fedha na wakuu
wa benki za taifa kutoka kundi la G20, wanatarajiwa kukutana kesho jumatano kwa
njia ya mtandao, ili kuchukua maamuzi.
Wakati huohuo shirika la
kimataifa la fedha-IMF, Jumatatu limesema kwamba jumuia ya kimataifa inatakiwa
kuongeza juhudi katika kukabiliana na athari za kiuchumi za janga la Covid-19.
IMF pia imetoa rasmi wito
kwa benki ya dunia kuendelea kutoa mkopo kwa mataifa ya Afrika yalioathiriwa na
janga la corona.
“Tutaendelea kuhamasisha ili hatua zaidi
zichukuliwe,” mkurugenzi wa IMF, Kristalina Georgieva, amesema
katika mkutano wa biashara wa mataifa ya Afrika kwa njia ya mtandao.
Ameongeza kuwa ataendelea
kuomba misaada zaidi ya pesa itolewe kwa nchi za Afrika.
Wiki iliopita, Georgieva, alisema kwamba IMF ilitoa mkopo wa dola billioni 26 kwa serekali za Afrika tangu litokee janga la virusi vya corona, lakini kutokana na uhaba wa mikopo ya sekta binafsi, bara la Afrika litakua na pengo la ufadhili wa dola billioni 345 ifikapo mwaka wa 2023.
EmoticonEmoticon