CORONA : Ujerumani Waongeza Makali Ya Amri Ya Kuvaa Barakoa

 

Kansela Angela Merkel na viongozi wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani wamekubaliana kuongeza makali ya amri ya kuvaa barakoa pamoja na kufungwa mapema maduka ya kuuza pombe katika maeneo yenye visa vingi vya COVID-19. 

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mkutano uliofanyika jana saa chache tangu Ujerumani iliporipoti maambukizi mapya  5,000 ya virusi vya corona katika kipindi cha saa 24, kiwango ambacho kikubwa kuwahi kushuhudiwa tangu katikati ya mwezi April.

Mapendekezo yaliyotolewa yanataka amri ya kuvaa barakoa ambayo tayari ni lazima ndani ya vyombo vya usafiri na maduka nchini Ujerumani pia itekelezwe kwenye maeneo ya umma yaliyo na msongamano katika wilaya zenye maambukizi makubwa ya  COVID-19.

Wakati hali nchini Ujerumani bado inatia moyo ikilinganishwa na mataifa mengine barani Ulaya, Kansela Merkel amesema ni muhimu kupunguza kwango cha maambukizi.

"Ninashawishika kuwa kile tutafanya au kutofanya katika siku na wiki zinazokuja kitakuwa muhimu kwa jinsi tutaondokana na janga hili. Kwa sabababu tunaweza kuona tarakimu za maambukizi ziko juu , baadhi ya maeneo kiwango kiko juu kabisa na pia tuna kiwango cha juu sana cha maambukizi katika baadhi ya majimbo ya Ujerumani ".

Miji mingi ya Ujerumani ikiwemo, Berlin, Cologne, Dusseldorf, Frankfurt na Munich imeshuhudia wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya corona hatua iliyolazimisha kurejeshwa kwa vizuizi vya kuzuia kusambaa virusi hivyo.


EmoticonEmoticon