Kura Zahesabiwa Guinea, Ghasia Zaripotiwa Ivory Coast

 

Nchini Ivory Coast, watu wawili wamefariki katika ghasia za uchaguzi, ikiwa ni wiki mbili kabla ya upigaji kura katika uchaguzi mkuu kwenye nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Kura zinaendelea kuhesabiwa nchini Guinea, baada ya uchaguzi mkuu wa jana jumapili, huku rais wa sasa Alpha Conde, mwenye umri wa miaka 82 akitarajiwa kushinda muhula wa tatu madarakani.

Polisi wameimarisha usalama kote nchini Guinea baada ya kutokea ghasia katika sehemu tofauti za nchi, kupinga hatua ya Conde kuwania muhula wa tatu.

Polisi wamesema kwamba shughuli ya kupiga kura ilifanyika katika mazingira yenye utulivu.

Uchaguzi huo umefanyika baada ya miezi kadhaa ya maandamano yaliyopelekea watu kadhaa kuuawa katika msako wa maafisa wa usalama dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakimpinga rais Alpha Conde.

Conde anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa kiongozi wa upinzani Cello Diallo na wagombea wengine 10. Tayari Diallo amedai kwamba huenda rais Conde akafanya udangayifu katika hesabu ya kura.

Kumekuwepo wasiwasi kwamba machafuko ya hivi karibuni yamechukua mkondo wa kikabila, rais Conde akishutumiwa kwa kusababisha migawanyiko kwa manufaa yake ya kisiasa, shutuma ambazo amekana.

Siasa za Guinea hugubikwa sana na ukabila. Rais Conde anatoka jamii ya Malinke huku mpinzani wake - Diallo, akitoka jamii ya Fulani.

Kuna wasiwasi mkubwa nchini Guinea kwamba huenda kukatokea ghasia baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi ambayo yatachukua mda kutolewa.


EmoticonEmoticon