Maambukizi Ya Corona Yaongezeka Ulaya Na Amerika Kusini

Ujerumani na Poland zimeweka upya karantini ili kudhibiti kuenea maambukizi ya virusi vya corona wakati idadi ya watu wanaoambukizwa ikiongezeka barani Ulaya, Karantini imewekwa upya katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin ambao ni maarufu kwa pilikapilika za usiku kama jitihada ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona. 

Migahawa na baa vitafungwa saa tano usiku, katika marufuku ambayo itadumu hadi Oktoba 31. Hatua kama hiyo imechukuliwa katika mji Frankfurt, lakini utekelezaji wake utaanza saa nne usiku.

Kukiwa na maambukizi ya zaidi ya watu 400 kwa siku mjini Berlin, ufungaji wa maeneo hayo ya biashara unahusu maduka yote isipokuwa maduka ya madawa na vituo vya kuuzia mafuta ingawa havitaruhusiwa kuuza pombe.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel tayari alikuwa ameonya siku ya Ijumaa kuwa maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi yataangaliwa kwa muda wa siku 10 kuona kama maambukizi yatapungua la sivyo hatua madhubuti zitachkuliwa ili kukabiliana na ongezeko la maambukizi na aliitaka miji mikubwa iongeze kasi ya kulidhibiti janga la corona. 

Katika nchi jirani ya Poland, viongozi wanawasisitizia watu wavae barakoa katika maeneo yote ya umma baada ya maambukizi mapya ya virusi vya corona kwa siku moja kupindukia watu 4,280 waliomabukizwa.


EmoticonEmoticon