Marekani Yadai Urusi Na Iran Zimejaribu Kuingilia Kati Uchaguzi

 

Maafisa wa idara ya ujasusi ya Marekani wamesema Urusi na Iran zimetumia taarifa za wapiga kura ili kuwatisha raia wa Kimarekani pamoja na kujaribu kuwafanya wapoteze imani na mfumo wa uchaguzi. 

Mkurugenzi wa idara ya ujasusi Marekani John Ratcliffe amesema Jumatano kwamba Urusi na Iran zimejaribu kuingilia kati uchaguzi wa rais unatarajiwa kufanyika rasmi Novemba 3, kwa lengo la kushawishi maoni ya wapiga kura.

Katika mkutano na waandishi habari, uliofanywa ghafla na kwa haraka, Ratcliffe amesema Iran na Urusi zimeweza kupata baadhi ya taarifa za usajili wa wapiga kura, na kuzitumia kusambaza taarifa za uwongo kwa wapiga kura waliojiandikisha ili kuhujumu demokrasia ya nchi hiyo.

Ameongeza kwamba maafisa wa serikali tayari walishagunduwa kwamba Iran imetuma barua pepe zinazolenga kuwatisha wapiga kura, kuchochea machafuko katika jamii na kuchafuwa jina la Rais Donald Trump.

Ratcliffe amevieleza vitendo hivyo kuwa ni vya mahasimu wanaotapatapa. Amesema Marekani itazishughulikia nchi zozote za kigeni zinazoingilia uchaguzi na kwamba maafisa wa ujasusi wameshaanza kujibu tishio hilo. Hata hivyo amewahimiza raia wa Marekani kuchukua tahadhari.

"Ukipokea barua pepe ya kutisha au ya ujanja, usiogope wala usiisambaze," amesisitiza Ratcliffe, na kumtaka kila Mmarekani ajilinde dhidi ya wale aliyowataja kuwa "wanawatakia mabaya." Ratcliffe amesema cha kufanya ni kutoruhusu juhudi hizo kuwa na athari iliyokusudiwa.


EmoticonEmoticon