Marekani Yaidhinisha Rasmi Dawa Ya Remdesivir Kutibu Corona

 

Mamlaka ya Marekani yameiidhinisha dawa aina ya remdesivir kuwatibu wagonjwa wa Covid-19 hospitalini.

Mamlaka ya chakula na dawa nchini Marekani (FDA) imesema Veklury, ambalo ni jina la dawa sokoni, imeweza kuwasaidia wagonjwa katika wastani wa siku tano wakati wa majaribio.

"Veklury ni dawa ya kwanza kuidhinishwa na mamlaka ya chakula na dawa kutibu ugonjwa wa corona," FDA ilieleza kwenye taarifa yake.

Wiki iliyopita Shirika la afya duniani (WHO) lilisema kuna ushahidi mdogo kuhusu ufanisi wa dawa ya remdesivir kumponya mgonjwa wa Covid 19.

WHO lilisema hii ni kutokana na utafiti wake, lakini mtengenezaji wa dawa hiyo kampun ya Gilead alikataa matokeo ya jaribio lililofanywa.

Remdesivir ilikuwa inaruhusiwa kutumika wakati wa dharura pekee nchini Marekani tangu mwezi Mei.

Hivi karibuni Rais Donald Trump alipatiwa dawa hiyo baada ya kupata maambukizi ya virusi vya corona.

Katika taarifa iliyotolewa na FDA , imesema dawa hiyo iliidhinishwa Alhamisi kwa ajili ya matumizi ya watu wazima na wenye umri wa miaka 12 na zaidi ambao wana kilo takribani 40, na wale ambao watakuwa wamelazwa kwa ajili ya kutibiwa corona.

"Leo hii kuidhinishwa kwa dawa hiyo imeambatanishwa na takwimu za matokeo ya majaribio kadhaa yaliofanyika kuthibitisha na kuona kuwa ni hatua kubwa muhimu ya kisayansi imefikiwa katika kukabiliana na janga la virusi vya corona," alisema msimamizi wa FDA Stephen Hahn.

Mamlaka hiyo imesema uamuzi huo uliungwa mkono na uchambuzi wa data kutoka kwa majaribio matatu ambayo yilijumuisha wagonjwa waliolazwa kutokana na Covid 19 na wale ambao hawakuathirika sana na Covid-19.

Utafiti mmojawapo umeonesha kuwa ''wastani wa muda wa kupona Covid-19 kwa kutumia dawa ya Veklury ilikuwa siku 10 tofauti na nyingine za placebo kuwa siku 15".


EmoticonEmoticon