Mchakato Wa Kuunda Tume Mpya Ya Uchaguzi Kenya Waanza

 

Sheria hiyo mpya, inaifanyia marekebisho sheria namba 9 ya mwaka 2011 ya tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesaini mswaada wa marekebisho ya sheria za tume ya uchaguzi nchini humo IEBC, na kuwa sheria, ili kufanikisha kuundwa kwa jopo la watu saba litakaloteua makamishna wapya wa tume hiyo kuunda nafasi za makamishna wanne waliojiuzulu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Hatua ya kuteua makamishna hao inaendelea kuibua hisia chungu nzima nchini humo kutoka kwa wanasiasa.

Sheria hiyo mpya, inaifanyia marekebisho sheria namba 9 ya mwaka 2011 ya tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC na inatoa mwongozo wa kubuni jopo litakalokuwa na jukumu la kutangaza, kuhoji na kufanikisha mchakato wa kuajiri makamishna wa uchaguzi ambao mwishowe watateuliwa na rais.

Hatua ya sheria hiyo kufanyiwa marekebisho inatoa udhaifu uliokuwepo kwenye sheria za uchaguzi nchini Kenya, ambapo hapakuwa na utaratibu wa kupata makamishna wapya iwapo waliopo wangejiuzulu kabla au baada ya uchaguzi.

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa sasa kubuni jopo hilo la watu saba kutoka kwa tume ya utumishi wa umma, tume ya huduma za bunge, tume ya maadhili na kupambana na ufisadi EACC, baraza la mawakili nchini Kenya LSK, miongoni mwa taasisi nyingine.


EmoticonEmoticon