Mdahalo Wa Mike Pence Na Kamala Harris

 

Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence na mgombea mwenza wa chama cha Democratic, Seneta Kamala Harris wameshiriki mdahalo wa nafasi ya makamu wa rais nchini Marekani, huku janga la virusi vya corona likitawala. 

Katika mdahalo huo uliofanyika Jumatano usiku kwenye mji wa Salt Lake, Harris ameikosoa serikali ya Rais Donald Trump kwa kushindwa kulishughulikia janga la virusi vya corona. 

Harris, 55 amesema watu wa Marekani wameshuhudia kushindwa vibaya kwa serikali katika historia ya nchi hiyo.

''Na ukweli ni huu, watu 210,000 wamekufa kwenye nchi yetu katika miezi kadhaa tu iliyopita. Zaidi ya watu milioni 7 ambao wameambukizwa ugonjwa huu, mmoja katika watu watano biashara yake imefungwa. 

Tunawaangalia zaidi ya watu milioni 30 ambao wamejiandikisha kukosa ajira miezi kadhaa iliyopita. Januari 28, makamu wa rais na rais waliarifiwa kuhusu hali ya janga hili. Walijua na walikaa kimya,'' alisisitiza Harris.

Kwa upande wake Pence, 61 amemkosoa Harris baada ya kuhoji iwapo chanjo ya corona iliyotangazwa chini ya utawala wa Trump kama inaweza kuaminiwa kutokana na shinikizo kali kwa rais kulidhibiti janga hilo. 

Pence amesema Trump amelipa kipaumbele suala la afya la Wamarekani. ''Taifa letu limepitia wakati mgumu sana mwaka huu. 

Lakini nataka kuwaambia watu wa Marekani kwamba, kuanzia siku ya kwanza kabisa, Rais Donald Trump ameweka mbele afya ya Wamarekani. 

Kabla ya kuwepo zaidi ya visa vitano Marekani, Rais Donald Trump alifanya kile ambacho hakuna rais mwengine yeyote wa Marekani aliyewahi kukifanya. Ndiyo maana alisitisha safari zote kutoka China, nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani,'' alifafanua Pence.


EmoticonEmoticon