Merkel Asisitiza Umuhimu Wa Diplomasia Kwenye Mzozo Wa Bahari Ya Mediterrania

Kansela wa Ujerumani Bibi Angela Merkel amerejea wito wake wa kutumia njia ya kidiplomasia kutatua mzozo wa eneo la mashariki ya bahari ya Mediterrania kati ya Uturuki, Ugiriki na Cyprus. 

Akizungumza kuelekea mkutano wa kilele wa viongozi wakuu wa mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya, bibi Merkel amesema uhusiano kati ya kanda hiyo na Uturuki ni muhimu akikumbusha kuwa Uturuki ni mwanachama wa Jumuiya ya NATO na inawahifadhi maelfu ya wakimbizi kwa niaba ya Ulaya. 

Wakati wa mkutano huo wa leo mjini Brussels suala la Uturuki litakuwa kitovu cha majadiliano na bibi Merkel amesema njia pekee ya kutuliza mivutano ni kutumia diplomasia. 

Wito kama huo umetolewa pia na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na waziri mkuu wa Bulgaria Boyko Borisov. Kwa upande wake waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis amesema japokuwa nchi yake ingependelea suluhu ya kidiplomasia, Uturuki itakabiliwa na vikwazo iwapo haitoonesha nia ya kupunguza mvutano.


EmoticonEmoticon