Mkataba Wa Kupiga Marufuku Silaha Za Nyuklia Waidhinishwa

 

Nchi 50 zimeidhinisha mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupiga marufuku silaha za nyuklia. Makubaliano hayo yatawezesha kuanza kutekelezwa kwa mkataba huo katika muda wa siku 90. 

Wanaharakati wanaopinga matumizi ya nyuklia wameisifu hatua hiyo lakini Marekani na mataifa mengine yenye nguvu yanayomiliki nyuklia wameupinga vikali mkataba huo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezipongeza nchi hizo 50 na amesifu kazi muhimu iliyofanywa na asasi za kiraia katika kuandaa mazungumzo na kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema mkataba huo utakaoanza kutekelezwa Januari 22 mwakani ni kilele cha harakati za ulimwenguni kote za kuwakumbusha watu juu ya matokeo mabaya kwa binadamu kutokana na matumizi ya silaha za nyuklia na pia ni harakati za kuwakumbuka watu walioathiriwa na milipuko ya nyuklia ikiwa ni pamoja na athari za majaribio ya silaha hizo, ambapo wengi wao ni miongoni mwa walioutetea mkataba huu. Guterres amesema mkataba huu unawakilisha hatua ya kujitolea inayolenga kuondolewa kabisa silaha za nyuklia, jambo ambalo linapewa kipaumbele na Umoja wa Mataifa.


EmoticonEmoticon