Papa Akosolewa Kuleta Mkanganyiko Kuhusu Ndoa Ya Wapenzi Wa Jinsia Moja

 

Mmoja wa wakosoaji wakubwa wa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema kauli yake ya hivi karibuni kuhusu wapenzi wa jinsia moja ni maoni binafsi ambayo hayastahili kuzingatiwa na Wakatoliki.

Kadinali Raymond Burke anayeonekana kuwa mhafidhina katika Kanisa Katoliki, ametoa tamko hilo siku chache baada ya Papa Francis kuonekana kuunga mkono wazo la kutambuliwa kisheria kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Kadinali Burke anasema pendekezo la Papa Francis la kutaka ndoa ya wapenzi wa jinsia moja kutambuliwa kisheria halijawashangaza wengi lakini maneno aliyotumia ndio yaliyowashangaza sana viongozi wa kidini na waumini wa Kanisa Katoliki.

Kadinali huyo ametaja matamshi ya Papa kama maoni ya kibinafsi na kwamba Kanisa katoliki na waumini wake hawatashurutishwa kutii msimamo wa kiongozi wa Kanisa hilo kuhusu suala la wapenzi wa jinsia moja.

Pia amesema viongozi wa kidini wa kanisa hilo wana jukumu la kutoa kile alichokitaja kama maelezo ya kina kuhusu suala hilo.

Kadinali Burke amesema imani rasmi ya kanisa Katoliki la Roma ni kuwa ndoa ya wapenzi wa jinsia moja hairuhisiwi na kwamba matamshi hayo ya papa yamewahuzunisha waumini wengi akidai kuwa matamshi ya papa hayaambatani na mafundisho ya Kanisa hilo.


EmoticonEmoticon