Papa Francis Akaataa Kuonana Na Waziri Wa Mambo Ya Nje Wa Marekani

Vatican imemkatalia waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo kuonana na Papa Francis.


Kiongozi huyo wa juu wa Kanisa Katoliki ameelezwa kuwa hawapokei wanasiasa wakati wa kipindi cha uchaguzi.

Hatua hiyo inaongeza hali ya mzozo wa kidiplomasia baada ya kauli ya Bwana Pompeo kuhusu China na Kanisa Katoliki.

Vatican ilimshutumu Pompeo kuwa anajaribu kutumia suala hilo kuvutia wapiga kura wa uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba nchini Marekani.

Katika makala ya mwanzoni mwa mwezi Septemba, Bwana Pompeo alisema kanisa Katoliki linapoteza ''mamlaka yake ya kinidhamu'' kwa kufanya makubaliano mapya na China kuhusu uteuzi wa maaskofu.

Donald Trump anapata uungwaji mkono kutoka kwa mashirika ya kidini ya kihafidhina, pamoja na wapiga kura wa Kikatoliki wa kihafidhina, ambao wengine wanadhani Papa Francis ni mtu mwenye uhuru sana.

Makundi ya haki za binadamu yanasema kuwa Wakatoliki wengi nchini China wanateswa kwa kuahidi utii kwa Papa badala ya chama rasmi cha Wakatoliki nchini China.


EmoticonEmoticon