Raisi Wa Marekani Trump Arejea Ikulu Huku Akipuuzia Corona

 

Rais wa Marekani Donald Trump amerejea kwa kishindo katika Ikulu ya White House kuendelea na tiba ya virusi vya corona baada ya kulazwa hospitali kwa siku tatu.

Rais alitoa barakoa yake katoka roshani ya White House, ambako wafanyakazi kadhaa na washauri wake walipatikana na virusi hivi karibuni.

"Najihisi vyema sana!" Bw. Trump awali aliandika katika Twitter yake."Usiogope Covid. Usiache itawale maisha yako."

Zaidi ya watu milioni 7.4 wamethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Covid-19 nchini Marekani. Virusi vya ugonjwa huo vimewaua takriban Wamarekani 210,000.

Maswali bado yanaibuliwa kuhusu ugonjwa wa Bw. Trump baada taarifa kinzani kutolewa wikendi iliyopoti kuhusu hali yake. Ukubwa wa mlipuko wa virusi katika Ikulu ya White House bado unaendelea kuwa kitendawili.

Akiwa amevalia suti , tai na barakoa, Bw.Trump alitoka nje ya Hospitali ya kitaifa ya kijeshi ya Walter Reed mjini Washington DC Jumatatu usiku akikunja ngumi na kuinua mkono juu.

Asanteni sana," alisema, akipuuza maswali kutoka kwa wanahabari, akiwemo mmoja aliyemuuliza: "Una uhakika hutasambaza virusi bila kujua bwana Rais?"

Baada ya safari fupi ya helikopta, Bw.Trump alipigwa picha akiwa peke yake kwenye roshani ya Truman katika Ikulu ya White House. Alivua barakoa, kisha akainua juu kidole gumba na baadae kupiga saluti ya mtindo wa kijeshi.

Saa chache baadae, aliweka ujumbe kwenye Twitter kama ishara kwamba anajiandaa kurejea kwenye msururu wa kampeni.

Muda mfupi kabla ya kuondoka hospitali, aliandika ujumbe kwenye Twitter yake na kusema: "Nitarudi kwe kampeni hivi karibuni!!! Taarifa feki zinaonesha kura feki za maoni."

Bw.Trump anagombea muhula wa pili madarakani na atakabiliana na mpinzani wake wa chama cha Democratic Joe Biden chini ya mwezi mmoja katika uchaguzi mkuu wa urais.


EmoticonEmoticon