Shirika La Afya Duniani Lasema Kuna Matumaini Ya Kupata Chanjo Ya Corona Mwishoni Mwa 2020

Kuna matumaini kwamba chanjo yenye ufanisi dhidi ya virusi vya corona itakuwa tayari mwishoni mwa mwaka huu, Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ulimwengu unahitaji kutumia "rasilimali zote zilizopo" kumaliza ugonjwa huo, ikiwemo kupata chanjo.

"Kuna matumaini mwishoni mwa mwaka huu kwamba tunaweza kuwa na chanjo, kuna matumaini ," Dkt Tedros alisema Jumanne mwishoni mwa mkutano wa siku mbili wa bodi kuu ya WHO.

Hivi sasa, kuna karibu chanjo 40 tofauti kwenye majaribio - pamoja na ile inayotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford ambayo tayari iko katika hatua ya juu ya majaribio.

Lakini Dkt Tedros hakufafanua ni chanjo gani ambayo alidhani itapatikana mwishoni mwa mwaka.

Mpango wa WHO unakusudia kuzipa nchi fursa sawa za chanjo tisa, mara tu wanapopewa leseni na kupitishwa.

Hatahivyo, wanasayansi wameonya kuwa chanjo haitarudisha maisha kuwa ya kawaida kama ilivyozoeleka, kwani inaweza kuchukua miezi kuzalishwa, kusambazwa na kusimamiwa kwa kiwango kikubwa.

Kwa nini chanjo ya virusi vya corona ni muhimu?

Virusi husambaa kirahisi, na watu wengi duniani wako hatarini kupata maambukizi. Chanjo itatoa kinga kwa kuimarisha mfumo wa kinga utakaowezesha kupambana na virusi hivyo kutougua.

Hatua hii itafanya kuondolewa kwa amri za marufuku ya kutotoka nje, na kulegezwa kwa masharti ya kutochangamana.


EmoticonEmoticon