Sumu Ya Novichok Yakutwa Kwenye Sampuli Za Navalny

 

Ujerumani imesema Shirika la Kimataifa la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kemikali, OPCW limethibitisha kwamba sampuli zilizochukuliwa kwa kiongozi wa upinzani wa Urusi, Alexei Navalny zinaonesha kuwa alipewa sumu. 

Msemaji wa Kansela Angela Merkel, Steffen Seibert amesema shirika hilo lilifanya uchunguzi wake na limekubaliana na matokeo ambayo tayari yalitolewa katika maabara za Ujerumani, Sweden na Ufaransa. 

Navalny mkosoaji mkubwa wa Rais wa Urusi, Vladmir Putin alipelekwa Ujerumani siku mbili baada ya kuugua Agosti 20 wakati akiwa safarini kwenye ndege nchini Urusi.

Duru za OPCW zimeeleza kwamba sampuli za damu na mkojo zimeonesha kuwa na kemikali ya ''cholinesterase inhibitor'' ambayo ni sawa na sumu ya Novichok inayoathiri mishipa ya fahamu, iliyopigwa marufuku mwaka 2019. 

Seibert amesema uchunguzi huo unathibitisha kwa mara nyingine tena kwamba Navalny alikuwa mwathirika wa shambulizi la kemikali ya Novichok. Amesema Ujerumani inarudia wito wake kwa Urusi kuchunguza kikamilifu na kueleza kile kilichotokea kwa Navalny.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Fernando Arias amesema matokeo hayo yanatia wasiwasi mkubwa na kwamba matumizi ya silaha za kemikali kwa mtu yeyote ni kinyume na kanuni za sheria zilizoanzishwa na jumuia ya kimataifa.


EmoticonEmoticon