Tetemeko Kubwa Laipiga Pwani Ya Uturuki

 

Tetemeko lenye ukubwa wa 7 katika kipimo cha Richter limeipiga pwani ya magharibi ya Uturuki, na ripoti za awali zinaarifu kuhusu uharibifu wa majengo, lakini haijajulikana ikiwa mtu yeyote amepoteza maisha. 

Kitovu cha tetemeko hilo lililosikika hadi mji mkuu wa Ugiriki, Athens, kilikuwa karibu na mji wa kitalii wa Izmir wenye wakaazi wapatao milioni 3. Waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki Suleyman Soylu amesema wamepata taarifa kuhusu majengo sita yaliyoporomoka katika mkoa wa Izmir. 

Kulingana na waziri wa mazingira wa Uturuki, Murat Kurum, watu kadhaa bado wako chini ya kifusi cha majengo yaliyoharibiwa. Shirika la Marekani la uchunguzi wa kijiolojia limesema tetemeko hilo limerekodiwa umbali wa kiomita 14 kutoka mji wa Neon Karlovasion katika kisiwa cha Samos katika bahari ya Aegean. 

Kupitia mtandao wa twitter, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ameahidi msaada wa serikali kwa wale watakaouhitaji.


EmoticonEmoticon