Trump, Biden Kwenye Mdahalo Mwengine Usio Rasmi

 

Wagombea wakuu wa urais nchini Marekani, Donald Trump wa Republican na Joe Biden wa Democratic, wamejitokeza katika vituo viwili tafauti vya televisheni, kila mmoja akimtuhumu mwenzake juu ya siasa za ndani na za nje. 

Katika kile kinachoonekana kama mdahalo baina yao, vituo viwili hasimu vya NBC na ABC nchini Marekani viliwaalika wagombea hao mahasimu pia kwa wakati mmoja kwa mahojiano ambayo yalirushwa moja kwa moja na kwa wakati mmoja usiku wa Alkhamis (Oktoba 15). 

Kwa wengi, mahojiano hayo yamechukuliwa kama duru ya pili ya mdahalo wa uso kwa macho kati ya Trump na Biden, ambao awali ulikuwa umepangwa kufanyika jana, lakini Trump akajitowa baada ya waandaaji kuamuwa ufanyike kupitia mtandao, kufuatia Trump kuuguwa COVID-19 wiki mbili zilizopita. 

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha ABC mjini Philadelphia, Biden alisema Trump hajayachukulia maradhi hayo, yashayoangamiza Wamarekani zaidi ya 217,000, kwa umakini zaidi.

"Maneno ya rais yana uzito mkubwa, ama yakiwa mazuri au mabaya. Na pale rais anapokuwa havai barakowa ama anawafanyia dhihaka watu kama miye ambao tunavaa barakowa muda mrefu, utaona watu wanasema kwamba kumbe barakowa sio muhimu kiasi hicho," alisema mgombea huyo wa Democratic ambaye anaongoza kwenye kura za maoni.


EmoticonEmoticon