Umoja Wa Ulaya Una Wasiwasi na Hatma Ya Usitishaji Mapigano Nagorno Karabakh

 

Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi wake kuhusiana na ripoti za ukiukaji makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya mataifa jirani yaliyo hasimu ya Armenia na Azerbaijan yanayowania udhibiti wa jimbo la Nagorno Karabakh. 

Taarifa iliyotolewa na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Jossep Borell, imesema kanda hiyo inatiwa shaka na operesheni za kijeshi zinazoendelea ikiwemo zinazohujumu maeneo ya makaazi na kuwalenga raia.

Taarifa hiyo Borell imetolewa baada ya kuvunjika kwa sehemu fulani makubaliano ya kusitisha mapigano baada ya kuzuka upya kwa makabiliano huku kila upande ukiulaumu mwingine kuhusiana na kilichotokea.

Borell amesema Umoja wa Ulaya unatoa wito kwa Armenia na Azerbaijan kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo chini ya upatanishi wa kundi  liitwalo OSCE Minsk linaloongoza juhudi za kumaliza mzozo wa Karabakh.

Pande hizo mbili zilifikia makubaliano ya kusitisha mapigano, kubadilishana wafungwa na miili ya wale waliouwawa katika mapambano ya wiki mbili kuwania udhibiti wa jimbo la Nagorno Karbakh.


EmoticonEmoticon