Chama Cha CDU Kumchagua Mrithi Wa Merkel Januari

 

Katibu Mkuu wa chama tawala cha Christian Democratic CDU nchini Ujerumani Paul Ziemiak ametangaza kuwa chama hicho kimeamua kufanya mkutano katikati ya mwezi Januari mwaka ujao kumchagua kiongozi mpya. 

Baada ya mazungumzo ya kina, wagombea watatu wa nafasi hiyo wameitaka bodi ya utendaji ya chama hicho kufanya mkutano huo Januari. 

Wagombea hao ni mfanyabiashara wa zamani na kiongozi wa CDU bungeni Friedrich Merz, Waziri mkuu wa jimbo la North-Rhine Westphalia Armin Laschet na mtaalam wa masuala ya mambo ya nje katika chama hicho Norbert Roettgen.

Mkutano huo wa wanachama 1001 ulikuwa umepangiwa kufanyika mwezi Disemba 4 ila uliahirishwa Jumatatu kwa sababu idadi ya maambukizi ya virusi vya corona inaongezeka Ujerumani na majimbo ya nchi hiyo yameweka vikwazo vipya.

Kuahirishwa kwa mkutano huo kulizua mgawanyiko baina ya wagombea hao watatu huku Friedrich Merz akiwatuhumu baadhi ya watu katika uongozi wa chama hicho kumpinga asiuchukue wadhfa huo.


EmoticonEmoticon