EU Kuzishinikiza Poland Na Hungary Kuhusu Hatma Ya Bajeti

 

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesema wanaongeza juhudi za kuwashawishi wenzao wa Hungary na Poland kuondoa pingamizi la  kuidhinishwa bajeti ya Umoja wa Ulaya na mpango wa uokozi wa uchumi wa kanda hiyo. 

Muda mfupi baada ya mkutano wa viongozi wa kanda hiyo uliofanyika kwa njia ya mtandao, kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema wataendelea kutafuta jibu la msuguano uliojitokeza ambao unatishia juhudi za kanda hiyo kukabiliana na janga la virusi vya corona.

Poland na Hungary zikiungwa mkono Slovenia zilitumia kura ya turufu kuzuia bajeti ya dola Trilioni 2.1 ya Umoja wa Ulaya wakipinga masharti yanayotaka nchi wanachama kuzingatia misingi ya utawala wa sheria kabla ya kupata fedha hizo.

Bibi Merkel ambaye nchi yake ni mwenyekiti wa zamu wa Baraza la Umoja wa Ulaya amesema mkwamo uliojitokeza ni tatizo kubwa na kwamba ni vigumu kutabiri mbinu za kupatikana ufumbuzi lakini amezitaka nchi wanachama kutoa nafasi ya masikilizano.

"Hii inamaanisha kuwa tumeshindwa kupeleka nyaraka mbele ya Bunge la Ulaya na hakuna kura itakayopigwa wiki inayokuja, na kwamba tunaendelea na mazungumzo na Poland na Hungary kuona kipi tunaweza kufanya kuhakikisha makubaliano yanafikiwa hapa." amesema Merkel.


EmoticonEmoticon