Kansela Angela Merkel Ampongeza Joe Biden, Ahimiza Ushirikiano Mpya

 

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amempongeza rais mteule wa Marekani Joe Biden kwa ushindi wake na kuutaka Umoja wa Ulaya na Marekani kushirikiana. 

Merkel amekiri pia kwamba Umoja wa Ulaya unastahili kuweka juhudi zaidi katika suala la usalama wake. Merkel amemzungumzia vyema Biden akimtaja kuwa kiongozi mwenye uzoefu ambaye anaifahamu vyema Ujerumani na Ulaya kwa ujumla. 

"Marekani na Ujerumani kama sehemu ya Umoja wa Ulaya zinastahili kushirikiana katika kukabiliana na changamoto kubwa zinazotukumba. 

Bega kwa bega tukabiliane na janga la virusi vya corona, tupambane na ongezeko la joto duniani na athari zake pamoja na kushirikiana katika vita dhidi ya ugaidi na tunastahili pia kusimama pamoja kwa uchumi wa wazi wa dunia na biashara huria kwa sababu huu ndio msingi wa maendeleo kwetu sote.

"Kansela huyo wa Ujerumani pia amesema makamu wa rais mteule Kamala Harris ni mfano mwema kwa watu wengi na kwamba anasubiri kwa hamu kufanya kazi na wote wawili, Biden na Harris.