Majaribio Ya chanjo Dhidi Ya Corona Yaanza Kenya

Kundi la kwanza la watu nchini Kenya wamejitolea kushiriki majaribio ya chanjo dhidi ya virusi vya corona iliyotengenezwa Uingereza.

Ni sehemu ya juhudi za kimataifa kupima ufanisi wa chanjo iliotengenezwa na chuo kikuu cha Oxford na kampuni ya kutengeneza dawa, Astra-zeneca.

Watu 14 waliojitolea, wengi wao wakiwa wafanyakazi wa afya, ndio wanashiriki kwenye jaribio la chanjo dhidi ya covid 19 nchini Kenya.

Awamu ya kwanza ya jaribio la chanjo hiyo inaongozwa na kituo cha utafiti KEMRI-Welcome Trust research program, kinachopatikana Kilifi.

Mmoja wa watafiti wa kituo hicho Dr Samuel Sang, anasema wanataka kuhakikisha kwamba chanjo hiyo ni salama kwa wanainchi wa Kenya.

“Chanjo zilizogunduliwa na kuwa na mafanikio na salama kwa baadhi ya raia, haimanishi kwamba itakua na mafanikio kwa raia wote wa dunia. Kwa hiyo kulikua umuhimu wa kutathmini iwapo chanjo hiyo ni salama na inafaa kwa wakenya waliojitolea, kuhakikisha wakenya wanajitolea kwa wingi kwa ajili ya jaribio la chanjo hiyo, lazima jaribio hilo liwe na mafanikio.” Amesema Dr. Sang

Kwa mjibu wa shirika la afya duniani (WHO), kuna karibu majaribio 100 ya chanjo dhidi ya covid 19 yanayofanywa kwa binadamu katika awamu ya kwanza.

Credit:Voaswahili


EmoticonEmoticon