Matumaini Ya Ushindi Yanukia Kwa Joe Biden

 

Katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais nchini Marekani mgombea wa chama cha Democratik Joe Biden yumo njiani kufikia idadi ya kura za kumpeleka ikulu. Matumaini sasa ni makubwa kwa Biden baada ya kulichukua jimbo la Michigan. 

Wakati huo huo rais Trump na timu yake wanataka kwenda mahakamani kupinga hesabu za kura. 

Mgombea urais wa chama cha Demokratik Joe Biden anakaribia kufikia idadi ya kura zinazohitajika kumfungulia mlango wa kuingia ikulu ya Marekani. Wakati idadi kamili inayohitajika ni kura 270 za wajumbe maalumu, Biden ameshatia kibindoni kura 264.

Hata hivyo mshindani wake rais Donald Trump amepinga hesabu hizo. Kambi ya kampeni ya Trump imesema imewasilisha malalamiko ya kisheria ili kusitisha kuhesabiwa kura za kwenye jimbo la Pennsylvania baada ya kutoa malalamiko juu ya hesabu za kura kwenye majimbo ya Michigan na Wisconsin.