Mkurugenzi Mkuu wa Shirika La Afya Duniani Ajiweka Karantini Kwa Hofu Ya Kuambukizwa Corona

 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuwa amejiweka karantini baada ya mtu mmoja aliyepatikana na virusi vya corona kumtaja kama mmoja wa watu wa karibu waliokutana naye.

"Nimeorodheshwa kama mmoja wa watu waliokutana na mtu aliyepatikana na #COVID19. Nipo vizuri, na sina dalili lakini nitajiweka karantini kwa siku zijazo, kwa mujibu wa taratibu za WHO, nikifanya kazi kutokea nyumbani," Tedros aliandika katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter, akiongeza kuwa ni muhimu kwa watu wote kufuata taratibu za kiafya zinazotolewa.

"Hivi ndivyo tutakavyovunja mnyororo wa maambukizi ya #COVID19, kuvizidi nguvu virusi na kulinda mifumo ya afya," aliandika Tedros.

Kauli ya Tedros inakuja wakati mataifa barani Ulaya kama vile Switzerland na Uingereza yakiingia katika kipindi kipya cha karantini kufuatia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.


EmoticonEmoticon