Mshirika wa
karibu wa Donald Trump amemsihi kuachana na jitihada zake za kuendelea kupinga
matokeo ya uchaguzi dhidi ya mpinzani wake Joe Biden.
Aliyekuwa
gavana wa New Jersey Chris Christie alikitaja kikosi cha sheria cha rais kama
"aibu kwa taifa".
Bwana
Christie amesema mara nyingi timu ya Trump imekuwa ikijadili wizi wa kura
"ikiwa nje ya mahakama, lakini wakifika mahakamani hawazungumzi lolote
kuhusiana na hoja hiyo".
"Nimekuwa
mfuasi wa Trump. Nimempigia kura mara mbili. Lakini uchaguzi una matokeo yake
na hatuwezi kuendelea kuonesha kwamba hakuna kilichotokea ilihali kinaonekana
wazi."
Bwana
Christie alikuwa gavana wa kwanza kumuidhinisha Trump kama mgombea wa urais
mwaka 2016. Pia alimsaidia rais katika maandalizi yake ya kukabiliana na
mpinzani wake Joe Biden kwenye mdahalo wa urais mapema mwaka huu.
Jumapili
wabunge wengine wa Republican walimtaka rais Trump kukiri kuwa ameshindwa.
Gavana
wa Maryland Larry Hogan ameiambia CNN Jumapili, hatua ya timu ya Trump
kuendelea kupinga matokeo ya uchaguzi "imeanza kuonesha chama cha
Republican kama kisichokuwa na maana".
Katika
ujumbe wa Twitter, Gavana Hogan amesema Bwana Trump aache "kucheza gofu na
kukubali kuwa ameshindwa".
Rais Trump amekataa kukubali kushindwa katika uchaguzi wa Novemba 3, akidai kulikuwa na wizi wa kura bila kutoa ushahidi wowote.
EmoticonEmoticon