NATO, Marekani Zatafautiana Kuwaondosha Wanajeshi Afghanistan

 

Wakati Marekani ikitangaza rasmi kuondosha idadi kubwa ya wanajeshi wake Iraq na Afghanistan, mkuu wa Shirika la NATO, Jens Stoltenberg, ameonya hatua hiyo inaweza kuigeuza Afghanistan kuwa "jukwaa la magaidi". 

Kauli ya Stoltenberg ilitolewa jana muda mchache kabla ya wizara ya ulinzi ya Marekani kutangaza kwamba itapunguza kwa kiasi kikubwa wanajeshi wake nchini Afghanistan, ambako wanasaidiana na kikosi cha NATO, na pia Iraq na kubakisha wachache sana baada ya takribani miaka 20 ya vita. 

Katibu mkuu huyo wa NATO alisema kundi la kigaidi ya ISIS linaweza haraka kurejesha dola ililolipoteza Iraq na Syria kwenye ardhi ya Afghanistan, endapo Marekani itaondosha wanajeshi wake bila mipango inayowashirikisha wengine.

Hilo ni tamko la nadra kwa mkuu huyo wa NATO, ambaye kawaida huwa hamkosoi hadharani Rais Trump wa Marekani, ambaye ndiye aliyechukuwa uamuzi huo.

Hapo jana, kaimu waziri wa ulinzi wa Marekani, Christopher Miller, aliwaambia waandishi wa habari kwenye makao makuu ya jeshi, Pentagon, kwamba wanajeshi 2,000 wataondoshwa nchini Afghanistan kufikia tarehe 15 mwezi Januari mwakani, huku wengine 500 wakirejeshwa kutoka Iraq, na hivyo kubakisha wanajeshi 2,500 tu kwa kila nchi.


EmoticonEmoticon